Monday, June 26, 2017

Nani anastahili kuwa mwana wa Mungu?

Bwana Yesu asifiwe!
Ndugu zangu wapendwa katika Kristo, swali hili ni gumu sana kulijibu kwa kutumia uzoefu. Njia rahisi ya kupata jawabu sahihi ni kwa kurejea katika misingi inayotupatia sifa za kuwa wana wa Mungu. Tuanze kwa kuangalia Biblia inasemaje katika kitabu cha Yohana 1:12 inasema
"Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake" mstari wa 13 unaongezea kusema "waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu".

Kwa hiyo katika kifungu hicho cha biblia tumeona mojawapo ya sifa anazostahili mtu ili kuwa mwana wa Mungu, ya kuwa ni lazima umpokee Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa Maisha yako ndipo utafanyika kuwa mwana wa Mungu. Kufanyika huku sio kwa kuzaliwa na wala si kwa mapenzi ya mtu bali Mungu Mwenyewe. Ni kwa wewe kuamini na kukiri ya kuwa Yesu ni Mwokozi wa maisha yako.

Vilevile katika kitabu cha Warumi sura ya nane mlango wa kumi na nne (Warumi 8:14) tunasoma "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu"
Kwahiyo, ukishampokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako yeye huingia ndani yako na kukaa nawe, kama asemavyo katika Ufunuo 3:20 ya kwamba " Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Huyo ndiye Roho aliyekuja baada yake kama Yesu alivyosema katika kitabu cha Yohana 16:13-14 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote. Huyu Roho ndiye aongozaye wana wa Mungu.
Ndugu mpendwa, mpaka sasa nafikiri utakuwa umepata walau taswira ya nani ni mwana wa Mungu. Kupitia ufahamu huo  ulioupata ni matumaini yangu kuwa umeijua nafasi yako kwa Mungu. Kwa Jina la Yesu Kristo nakuomba uchukue uamuzi sahihi wa kumtafuta Mungu ili ufanyike kuwa Mwana.
Mungu na akufanikishe.
AMINA

1 comment:

  1. Watu wengi duniani wanasumbuka wakikabiliana na changamoto za maisha kwa sababu mbele za Mungu wanaonekana ni watoto.
    Mtoto siku zote harithishwi mali.
    Jitahidi ndugu yangu utoke katika lindi hilo ili Bwana akuzukie.
    Amina

    ReplyDelete